Profile

Utangulizi

Wizara ya Uchukuzi iliundwa Disemba, 2010, baada ya kuitenganisha iliyokuwa Wizara ya Miundombinu na kuundwa Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Ujenzi. Wizara hii inasimamia sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa.

Wizara ya Uchukuzi inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sera za Kitaifa na Kisekta, Mikakati ya Kitaifa ambayo ni pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo (Vision 2025), Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA), Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (JAST), Sera na Sheria ya Uhifadhi wa Mazingira na malengo ya Kimataifa kama vile Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals- MDGs). Sera za kitaifa na kisekta ni Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya mwaka 2003 na Sera ya Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi (PPP Policy) iliyopitishwa mwaka 2010.

Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya IV (2005-2015), Wizara ya Uchukuzi pamoja na taasisi zake imepata mafanikio katika miundombinu na huduma za reli, bandari, usafiri wa anga na hali ya hewa.

Dira ya Sekta

Kuwa wizara inayooongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki katika utoaji wa huduma za uchukuzi na hali ya hewa zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Dhima

Kuwezesha kuwa na huduma na miundombinu ya uchukuzi ambazo ni salama,zinazotegemewa, zilizo na uwiano na ambazo zinakidhi mahitaji ya usafiri na uchukuzi katika kiwango bora kwa bei nafuu na zinazoendana na mikakati ya serikali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii zikiwa endelevu kiuchumi na kimazingira.

Muundo

Wizara ya Uchukuzi ina Idara 5 ambazo ni Idara za Utawala na Rasilimali Watu, Miundombinu ya Uchukuzi, Huduma za Uchukuzi, Sera na Mipango, Manunuzi na Usalama na Mazingira. Aidha, Wizara ina Vitengo 6 ambavyo ni Fedha na Uhasibu, Mawasiliano Serikalini, Ukaguzi wa Ndani, Huduma za Sheria na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Aidha wizara ina kitengo cha kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.

Taasisi za Sekta

Taasisi za Wizara ya Uchukuzi ni Kampuni ya Reli Tanzania(TRL),Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini(RAHCO), Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania(TAA). Aidha, taasisi zingine ni Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Kampuni ya Meli ya Tanzania na China (SINOTASHIP) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na vyuo vya mafunzo ambavyo ni Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Bahari Dar es salaam (DMI), Chuo cha Hali ya Hewa (Kigoma), Chuo cha Usafiri wa Anga Dar es Salaam (CATC) na Chuo cha Reli Tabora.

.