News

WIZARA NA TANROADS WAASWA

Posted On: Wednesday 26, July 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, na watendaji wake kupitia upya mkataba wa ujenzi waliokubaliana na mkandarasi atakayejenga barabara ya Mkiwa - Itigi- Makongorosi yenye urefu wa KM 57 kwa kiwango cha lami.

Akizungumza mkoani Singida katika sherehe za ufunguzi wa barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya KM 89.3, Rais Magufuli amesema kuwa shilingi Bilioni 104 kama gharama za ujenzi atakazopewa mkandarasi huyo ni nyingi sana ukilinganisha na urefu wa Kilometa za barabara hiyo, hivyo ni jukumu la Wizara kuona namna ya kupunguza gharama hizo ili kuokoa fedha za Serikali.

"Waziri na watendaji wako nataka mpitie gharama za ujenzi za mkandarasi huyu, haiwezekani kwa barabara yenye kilometa chache kujengwa kwa bei ya juu, lengo letu ni kuhakikisha barabara hii inajengwa kwa gharama zinazoeleweka na kwa wakati unaotakiwa", amesema Rais Magufuli.

Amemuagiza Waziri Mbarawa kujadiliana na mkandarasi huyo kwa kutumia fedha hizo kuendelea kujenga barabara ya kutoka Itigi-Chunya-Makongorosi mkoani Mbeya, endapo itashindikana basi Waziri apunguze fedha hiyo ili kuzuia uharibifu na matumizi mabaya ya fedha za Serikali ambazo zinatokana na kodi za wananchi.

Kwa upande wake, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumerahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka mkoa huo na mikoa ya jirani ya Tabora na Kigoma, hivyo kuchochea na kufungua fursa za kijamii na kiuchumi.

"Wananchi wa mkoa wa Singida sasa ni jukumu letu kuilinda na kuitunza barabara hii ili idumu kwa muda mrefu, kukamilika kwa barabara hii kuna umuhimu mkubwa kwenu katika kuinua uchumi wenu na Taifa kwa ujumla", amesema Prof. Mbarawa.

Barabara ya Manyoni - Itigi - Chaya yenye urefu wa KM 89.3 imejengwa na mkandarasi SinoHydro Cooperation kutoka China kwa gharama ya shilingi Bilioni 114.69 ambazo zimetolewa na Serikali kwa asilimia mia moja.