News

WAZIRI PROF. MBARAWA AZINDUA SAFARI ZA NDEGE KUTOKA KIA KUELEKEA DUBAI

Posted On: Saturday 16, December 2017

Serikali imesema itahakikisha inatoa ushirikiano kwa Shirika la Ndege la Dubai(Fly Dubai), kuhakikisha kwamba inafanya kazi zake vizuri za utoaji wa huduma za usafiri wa anga hapa nchini.

Akizungumza leo mkoani Kilimanjaro katika uzinduzi wa safari za ndege kutoka Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) kuelekea nchini Dubai, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa uzinduzi wa safari hizo utakuza sekta ya utalii na biashara mkoani humo na nchi kwa ujumla.

"Naamini kupitia uzinduzi huu uchumi wetu utakua kwani wafanyabiashara na watalii kutoka nchi mbalimbali wataweza kuongezeka zaidi sababu wamesogezewa huduma za usafiri wa ndege za kimataifa katika viwanja vya ndege vikubwa nchini", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ameuhakikishia uongozi wa shirika hilo la ndege kuwa hawatojutia uamuzi wao wa kuamua kusogeza huduma zao za usafiri katika uwanja huo kwani wafanyabiashara wengi na wananchi kutoka sehemu mbalimbali wamekuwa wakitumia uwanja huo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirika la ndege la Dubai, Sudhir Sreedharan, amesema kuwa kutokana na umuhimu na ubora wa uwanja huo wameamua kusogeza huduma zao kutokana na kuamini kuwa wageni wengi wa kimataifa wamekuwa wakitumia uwanja huo kwenda sehemu mbalimbali za vivutio vya utalii mkoani humo na mikoa ya jirani ya Arusha na Manyara.

"Kuna mambo mengi yametuvutia kuanzisha safari zetu katika uwanja huu, tunaamini hata soko letu la biashara litafanikiwa kwa kuongeza huduma hapa", amefafanua Makamu wa Rais.

Shirika la ndege la Dubai, sasa litatoa huduma za usafiri wa anga katika viwanja vya ndege vitatu kikiwemo kilichozinduliwa leo cha KIA na vile viwanja viwili vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa ndege wa Zanzibar vilivyokuwa awali.