News

WAZIRI PROF. MBARAWA AAGIZA CHUO CHA RELI TABORA KUANDAA WATAALAMU

Posted On: Sunday 16, July 2017

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa wito kwa uongozi wa Chuo cha Reli cha Tabora kuwajengea uwezo wanachuo ili kupata wataalamu wenye ujuzi, weledi, maarifa na uadilifu katika kusimamia mradi mkubwa wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge).

Waziri Prof. Mbarawa ametoa wito huo alipotembelea chuo hicho ambacho kinatoa mafunzo mbalimbali yahusuyo reli na kusisitiza ushirikishwaji wa wanachuo hao katika kusimamia ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), ili kuwajengea uwezo.

"Serikali inawategemea ninyi kuendesha Reli ya Kisasa kwa kuwa ujenzi wa reli ni kitu kimoja na usimamizi na uendeshaji ni kitu kingine", amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Amewataka wanachuo hao kusoma kwa bidii, kuwa waadilifu na wazalendo ili kuweza kuendesha Reli ya Kisasa (Standard Gauge) na Serikali itahakikisha kuwa inawapatia mafunzo kwa vitendo ya kutosha ili wawe na umahiri unaotakiwa.

Aidha, ameongeza kuwa Mkoa wa Tabora utakuwa ni kiungo muhimu cha Reli ya Kisasa kwani utaunganisha Mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Mwanza na nchi za jirani.

Prof. Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), utagharimu takribani shilingi Trilioni 16 hivyo kuwataka watanzania kutumia fursa hiyo ya kujipatia ajira na kufanya kazi kwa uzalendo.

Ujenzi wa reli ya kisasa utabadilisha maisha ya watanzania na raia wa nchi za jirani kwani utarahisisha huduma za usafiri wa abiria na uchukuzi wa mizigo kutoka Rwanda, Uganda na D.R.C Congo.

Naye, Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Reli cha Tabora, Bwana IsaacFundisha, amemshukuru Prof. Mbarawa kwa kutembelea Chuo hapo, kuzungumza na wanafunzi na kuonesha utayari wa Serikali wa kuwapatia wanachuo hao mafunzo kwa vitendo wakati wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo na wengine kupata fursa ya ajira.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi ya miundombinu iliyopo mkoani Tabora.