News

WAZIRI KAMWELWE ATAKA KASI UJENZI WA BARABARA MKOANI RUVUMA

Posted On: Wednesday 10, October 2018

IMEELEZWA kuwa kukamilika mapema kwa barabara za lami na madaraja ya kisasa katika mkoa wa Ruvuma kutauunganisha kirahisi na mikoa ya nyanda za juu kusini na nchi za jirani na hivyo kuhuisha uchumi wa wakazi wake.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe amesema hayo alipokagua ujenzi wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay KM 60 na kumtaka mkandarasi china Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO), anayejenga barabara hiyo kuikamilisha kwa wakati.

Amesema fursa za kilimo, uvuvi, usafirishaji na uchukuzi wa mazao na makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma zinahitaji barabara za lami na zenye uwezo wa kupitika wakati wote na kwa urahisi hivyo kukamilika kwa barabara za lami kwa wakati kutaleta ukombozi kwa wananchi wa mkoa huo.

“Viwanda vingi sasa vinatumia makaa ya mawe tena kwa kiwango kikubwa hivyo tunahakikisha usafiri katika mkoa huu unakuwa wa uhakika ili kuufungua na kuunganisha na mikoa mingine kwa njia fupina hivyo kuongeza biashara ya ndani kuvutia biashara na nchi za jirani”, amesema Mhandisi Kamwelwe.

Amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara za Ikuyufusi –Mkenda,Kitae-Lituhi KM 84.5, Lituhi –Mbamba Bay KM 112.5 na kukamilisha kwa wakati daraja la Ruhuhu linalounganisha mkoa wa Ruvuma na Njombe kupitia Ludewa ili kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi mkoani Ruvuma.

Amewataka wakazi wa wilaya za Mbinga na Nyasa kufanya kazi kwa bidii na kuchangamkia fursa za ujenzi wa barabara za lami, uwepo wa makaa ya mawe na uvuvi wa kisasa ili ziwaletee maendeleo.

Kuhusu ujenzi wa daraja la Ruhuhu unaojengwa na mkandarasi Lukolo, Waziri Kamwelwe ameelezea kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi huo na hivyo kuuagiza Wakala wa Barabara Nchini TANROADS kuangalia njia ya kumsaidia mkandarasi huyo kukamilisha kazi hiyo kabla ya mvua za masika.

Naye mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi, Isabela Chilumbaamemwomba Waziri Kamwele kuhakikisha barabara nyingi zinazoelekea mipakani zinaboreshwa ili kuvutia wafanyabiashara wa nchi jirani kwenda Ruvuma kununua bidhaa na hivyo kuongeza uchumi wa mkoa huo.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Ruvuma MhandisiLazeck Alinanusweamemhakikishia Waziri Kamwele kuwa ujenzi wa barabara za lamimkoani Ruvuma utasimamiwa kimkamilifu ili ubora wake uwiane na mahitaji na thamani ya fedha inayowekezwa.

Barabara za lkuyufusi- Mkenda, Kitai –Lituhi, Mbinga-Mbamba Bay na Mbamba Bay- Lituhi zikikamilika kwa lami licha ya kuuunga mkoa wa Ruvuma na Njombe zitaimarisha shughuli za kilimo, uvuvi na biashara ya makaa ya mawe na kuinua uchumi wa mkoa wa Ruvuma.