News

​ WAZIRI KAMWELWE ATAKA BOMBARDIER IANZE SAFARI ZA IRINGA MWEZI HUU

Posted On: Friday 05, October 2018

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe ameagiza kukutana mara moja kwa viongozi wakuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na Shirika la Ndege (ATCL) ili kukagua na kuamua lini katika mwezi huu ndege za Bombardier zitaanza safari zake mkoani Iringa.

Akizungumza mara baada ya kukagua uwanja uwanja wa ndege wa Nduli mkoani Iringa uliofanyiwa ukarabati katika njia ya kuruka na kutulia ndege Mhandisi Kamwelwe amesema anataka tathmini ya viongozi hao mapema kabla ya kuruhusu ndege za Bombardier kutumia uwanja huo na hivyo kuvutia watalii, kurahisisha huduma za usafiri na kukuza uchumi wa mikoa ya Iringa na Njombe.

“Licha ya uwanja huu kuwa katika mpango wa kupanuliwa ili ndege nyingi na kubwa ziweze kutua lakini kwa ukarabati uliofanywa hadi sasa nataka ndege za Bombedier zitumie uwanja huu ili kuvutia watalii wengi katika hifadhi ya Ruaha na kurahisisha huduma za usafiri wa anga katika mkoa wa Iringa”,amesema Mhandisi Kamwelwe.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha usafiri wa anga katika mkoa wa Iringa unaboreshwa sambamba na ujenzi wa barabaraiendayo katika hifadhi ya Ruaha ambapo KM 104 ujenzi wake utaanza hivi karibuni.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindoleamesema tayari mita 250 za barabara ya kurukia na kutulia ndege zimekarabatiwana hivyo kuuwezesha uwanja huo kuwa katika hali nzuri kwa sasa.

Mhandisi Kindole amesisitiza umuhimu wa uwanja wa ndege huo kuwa na uzio, kujengwa kwa lami barabara za kuingilia na kutoka uwanjani, kupanuliwa jengo la abiria na kuwepo kwa gari la zimamoto ili kuvutia ndege nyingi kuutumia uwanja huo na kukuza uchumi wa mkoa wa Iringa.

Naye Meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa Bi, Hanna Kibopile amemhakikishia Waziri Kamwelwe kuwa mkoa wa Iringa una abiria wengi wanaohitaji usafiri wa anga hivyo kuanza kwa safari za bombardier kutaongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa mikoa ya Iringa na Njombe.

Waziri Mhandisi Kamwelwe yuko katika ziara ya kukagua miundombinu ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano katika mikoa ya nyanda za juu kusini.