News

WAZIRI KAMWELWE AITAKA BODI TMA KUBUNI VYANZO VYA MAPATO

Posted On: Friday 29, November 2019

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameitaka Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania (TMA) kubuni vyanzo vipya vya mapato na kukusanya mapato kwenye vyanzo vyote ambavyo Mamlaka inatoa huduma ili kuifanya mamlaka kujiendesha na kuongeza pato la Taifa.

Waziri Kamwelwe ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati akizundua Bodi ya kwanza ya Mamlaka hiyo ambapo kabla ilikuwa Wakala na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea na taratibu za kuboresha maslahi yao kutokana na umumihu wa fani ya utabiri katika maslahi ya Taifa.

“Hakikisheni mnakusanya mapato kwenye maeneo yote mnayotoa huduma zenu zikiwemo usafiri wa Anga, majini, nchi kavu, kilimo na maeneo mengine, kwani fedha hizo mtazitumia kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa, pia mtaongeza pato la Taifa kwa kuchangia sehemu ya mapato kwenye mfuko wa Serikali”, Amesema Waziri Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe ameipongeza Mamlaka kwa kutumia wataalam wa mamlaka hiyo kubuni mifumo ya Tehama na kuitumia katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa ndani na nje ya nchi na kusisitiza taasisi nyingine zilizo chini ya sekta kuwatumia wataalam wa taasisi zao ili kuboresha utendjai kazi.

“Nimpongeze Mkurugenzi Mkuu kwa kuwatumia wataalam wa taasisi yenu kwa kubuni mifumo ya Tehama na kuitumia kurahisisha utoaji wa taarifa hizo, ni vizuri sasa kwa taasisi nyingine ziige utaratibu huu kwa kuwatumia watumishi wenye fani mbalimbali kubuni program tumishi zitakazorahisisha utendaji kazi”, amesisitiza Waziri Kamwelwe.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Agnes Kijazi, amesema kwa sasa usahihi wa taarifa za hali ya hewa umeongezeka kutoka asilimia 75 mpaka 87 na kuwezesha mamlaka hiyo kupata tuzo kitaifa na kimataifa katika utoaji taarifa hizo.

Dkt Kijazi, aimeshukukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye vifaa ambapo mpaka sasa Serikali imeshawekeza kwenye ujenzi wa rada 5 ambapo ujenzi wake unaendelea nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mpya wa bodi hiyo Dkt. Buruhani Nyenzi, amemhakikishia Waziri Kamwelwe, kutumia taaluma zao kuboresha utendaji wa Mamlaka ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuahidi kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi yote ya hali ya hewa.

Wajumbe walioteuliwa kuunda bodi hiyo ni Dkt Buruhani Nyenzi (Mwenyekiti wa Bodi hiyo), Dkt Makame Omary ambaye ni Makamu Mwenyekiti na Wajumbe ni Kapteni Large Temba, Robert Sunday, Marystella Mtalo, Jane Kikunya pamoja na Mhandisi Aron Kisaka.