News

WAZIRI KAMWELWE AITAKA BODI KUSIMAMIA MAPATO

Posted On: Tuesday 11, February 2020

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inajiendesha kwa faida na kuchangia pato la Serikali kwani imekuwa ikijiendesha kwa hasara kwa miaka mingi.

Ametoa kauli hiyo mara baada ya kuzindua bodi hiyo jijini Mwanza na kueleza kuwa Serikali imewekeza vya kutosha kwakufanya ukarabati wa meli 3 na ujenzi wa meli mpya moja kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 1000 na mizigo tani 200.

“Uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa kampuni hii ni mkubwa kwani imetoa fedha za ukarabati wa meli na kuonyesha umuhimu wa kufufua kampuni hii imewalipa mshahara wa miezi 27 alafu kampuni ijiendeshe kwa hasara. Wajumbe wa bodi msiruhusu jambo hili kujirudia” Amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.

Waziri amesema kuwa lengo la kuchelewa kuteua wajumbe wa bodi ni ilikuwa ni pamoja na kujiridhisha kama wajumbe walioteuliwa wataweza kutatua changamoto zinazoikabili kampuni hiyo.

Aidha, Waziri Kamwelwe amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko kukaa na menejimneti ya kampuni hiyo ili kukamilisha zoezi la kuwapa matenki ya kuhifadhia mafuta yaliyopo katika bandari ya Mwanza North ili kupunguza gharama za uendeshaji ambapo asilimia Zaidi ya sitini ya matumizi ni mafuta ya meli.

Wakati huo huo Waziri Kamwelwe ameuagiza uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya ukarabati wa reli inayoingia bandarini hapo ili kurahisisha uingizaji wa mafuta.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli, Bw. Eric Hamiss ameishukuru Serikali kwa kuwekeza fedha nyingi ambazo zimeongeza utendaji kazi wa kampuni hiyo kutoka kutumia meli moja mpaka meli nne kwa kanda ya ziwa, kulipa madeni ya mishahara kwa watumishi na kulipa mishahara ya miezi 27 mbele, ujenzi wa meli mpya ya kisasa na kuwezesha deni kupungua kutoka bilioni 7 mpaka bilioni 4.

Hamis amemuhakikishia Waziri huyo kuwa kampuni hiyo itaendelea kuboresha utendaji kazi kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, kusimamia hesabu ili kuendelea kupata hati safi katika mahesabu yake.

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Kampuni hiyo, Profesa Zacharia Mganilwa ameitaka menejimenti na watumishi kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano kwa kufanya kazi kwa bididi na ubunifu na kumuhakikishia Waziri Mhandisi kusimamia kampuni hiyo ili iweze kuongeza mapato.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 21 Januari 2020 alimteua Profesa Zacharia Mganilwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Kampuni hiyo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aliwateua Dkt. Elizabeth Mwakasangula, Dkt. Tumaini Gulumo, Bi Julliete Nyerere, Bw. Bantu Mgalla na Bw. Michael Masinda kuwa wajumbe wa bodi hiyo.