News

WATU KUMI NA MOJA WASHIKILIWA KUHUJUMU MIZANI

Posted On: Friday 17, January 2020

Imeelezwa kuwa mpaka sasa zaidi ya watu tisa wameshikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini kwa mahojiano baada ya kubainika kufanya vitendo viovu katika mizani hapa nchini.

Ameyasema hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia Sekta ya Ujenzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Sekta hiyo, Arch. Elius Mwakalinga, katika ufunguzi wa mkutano wa Baraza hilo lililofanyika mkoani Iringa ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa Wizara itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wasafirishaji ambao wataokiuka sheria ya udhibiti wa uzito wa magari ya mwaka 2016.

“Toka tuanze mfumo tumeshawashika watu 11 na bado tunaendelea kufuatilia ili tuwashike zaidi na hatua kali zitachukuliwa ili kukomesha vitendo vya uhujumu katika mizani”, amesisitiza Arch. Mwakalinga.

Mwakalinga amesema kuwa hatua hiyo imetokana baada ya Sekta hiyo kuanzisha utaratibu wa kufuatilia utendaji kazi wa mizani kwa saa ishirini na nne kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na kamera za CCTV kwa ajili ya kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa mizani na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Aidha, amefafanua kuwa Sekta imeanza mchakato wa ununuzi wa gari kwa ajili ya mfumo wa kusimamia miundombinu ya barabara kwa ufanisi, weledi na kwa gharama nafuu ikiwa na lengo la kuhakikisha kazi za ukaguzi wa barabara zinafanywa kwa ufanisi.

“Gari hilo ambalo litakuwa la kisasa na lenye mionzi itakayowezesha kukagua mtandao wote wa barabara hapa nchini ndani ya mwezi mmoja na kutoa majibu ya ubora na mapungufu ya barabara kuanzia hatua za awali za ujenzi hadi mradi utakapokamilika”, amesema Arch. Mwakalinga.

Katika kuhakikisha Tanzania inapata wakandarasi wazawa na wenye uwezo wa kujenga na kusimamia miradi mikubwa nchini kwa lengo la kuchangia maendeleo ya Taifa pia Sekta hiyo imekwisha peleka wataalamu 33 kwenye miradi mbalimbali nchini ili kuleta mapinduzi katika Sekta za Ujenzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ally Hapi, ameipongeza Sekta hiyo kwa kuandaa baraza hilo na mikakati mbalimbali ya kimaendeleo ambayo ina lengo la kukuza uchumi wa nchi.

“Nichukue fursa hii kuipongeza Sekta hii kwa kuandaa baraza hili na mikakati ya kiutekelezaji ambayo mmejiwekea, naamini kupiti mipango yenu nchi hii itapata wataalamu wengi zaidi ambao wataweza kusaidia kuleta maendeleo ya Taifa hili”, amesema Hapi.

Ameipongeza Sekta hiyo kwa kuchagua mkoa huo kwa kufanya baraza hilo na kuwaalika kutembelea vivutio vilivyopo katika mkoa wake ili kuhamasisha utalii wa ndani na kuongeza pato la Taifa.

Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi la siku mbili ambalo lina wajumbe zaidi ya 100 limekutana kupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa sekta, mafanikio pamoja na changamoto za sekta hiyo ili kufikia maamuzi yanayohusu sekta ya ujenzi na taasisi zake.