News

WANANCHI WA CHILONWA, DODOMA WAIOMBA SERIKALI KUJENGA DARAJA.

Posted On: Tuesday 06, June 2017

Wananchi wa kata ya Chilonwa, wilaya Chamwino mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kujenga daraja la Chilonwa lililopo katika kata hiyo ili kutatua kero ya usafiri kwa wananchi hao na maeneo jirani hususan katika kipindi cha masika.

Wakieleza kero yao kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, wananchi hao wamesema wanaamini kuwa ujio wa Naibu Waziri huyo katika kata yao kutaleta ufumbuzi wa kero hiyo.

"Tunaamini sasa tutapata mwarobaini wa daraja hili kwani tatizo hili ni la muda mrefu, siku hadi siku daraja linakuwa fupi kutokana na kufukiwa na mchanga na hivyo hupelekea maji kujaa darajani hapa kipindi cha masika na watu kushindwa kuvuka", amesema mmoja wa wananchi hao.

Aidha, wananchi hao wamemwomba Naibu Waziri huyo kurekebisha daraja hilo kwa kulijenga juu zaidi ili kupitisha maji na kupitika katika vipindi vyote vya mwaka kutokana na kwamba lililopo sasa lipo chini zaidi mara baada ya kufukiwa na mchanga.

Wananchi hao wameeleza masikitiko yao kwa Naibu Waziri huyo hususan katika kipindi cha masika ambapo wamesema hutumia kiasi cha shilingi elfu kumi kuvushwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wengine hupoteza maisha wakiwa wanavuka.

Sambamba na hilo wananchi hao wamependekeza kuwa ujenzi wa daraja hilo uhusishe wataalamu waliobobea na ambao watahakikisha daraja hilo linakamilika mapema na kwa viwango.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ngonyani, amewataka wananchi hao kuacha tabia ya kufanya shughuli za kibinaadamu kama kilimo katika njia ya mto kwani hali hiyo hupelekea udongo kumung’unyuka na hatimaye mchanga kufunika daraja.

Amemtaka Mbunge wa jimbo la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga, kwa kushirikiana na viongozi wa kata na kijiji kuhamasisha wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinaadamu kando ya mto.

Amefafanua kuwa Wizara yake kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoaniDodoma itahakikisha kwanza ina utengeneza mto huo kwa kuelekeza maji yote katika mto.

Naye, Mbunge wa jimbo la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga, amempongeza Naibu Waziri huyo kwa kutembelea jimboni hapo na kuahidi kuwasimamia wananchi wake katika kulinda miundombinu hiyo.

Naibu Waziri Ngonyani leo ametembelea na kukagua Daraja la Chilonwa, wilayani Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni kutekeleza ahadi yake ya kutembelea na kukagua daraja hilo kwa Mbunge wa jimbo la Chilonwa, Mhe. Joel Makanyaga.