News

WAHANDISI WA UJENZI WAHAMASISHA USOMAJI WA SAYANSI LINDI.

Posted On: Wednesday 20, September 2017

Wahandisi wa kike wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara wamewataka wanafunzi wa kike mkoani Lindi kutokata tamaa na badala yake kutumia mbinu mbadala za usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati ili kuweza kufikia malengo yao.


Akizungumza kwa niaba ya wahandisi hao katika shule ya Sekondari ya Mahiwa kata ya Nyingo mkoani Lindi, Mhandisi Liberatha Alphonce , amesema kuwa ufaulu wa masomo hayo utategemea ufanyaji wa maswali na mazoezi ya kujipima mara kwa mara ambayo yatajenga uelewa na hivyo kupelekea ufaulu mzuri.

"Sayansi si ngumu kama ambavyo mnadhani, hakikisha unapanga ratiba yako vizuri na kuzingatia yale unayofundishwa na walimu darasani, kamwe usikate tamaa kwani ndoto zako zitatimia endapo ukifanya juhudi", amesema Mhandisi Alphonce.

Aidha, wahandisi hao wamefafanua kuwa sekta hiyo bado ina uhaba wa wataalamu wa kike hivyo inahitaji wanafunzi kusoma masomo hayo ili kuongeza idadi ya wataalamu hao na kuweza kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mahiwa Bi. Emaculathe Mallya, kwa niaba ya walimu wenzake ameishauri Serikali kutembelea mara kwa mara shule mbalimbali nchini ili kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Ameongeza kuwa ipo haja ya Serikali kuandaa vipeperushi vitakavyobainisha dhana na faida za masomo hayo ili kumsaidia mwanafunzi kupata uelewa wa namna ya kupambana na soko la ushindani mapema.

Naye, Fundi Sanifu wa maabara ya shule hiyo, Mwalimu Kili Mbwanji, ameiomba Serikali kuongeza walimu wa kike wa sayansi shuleni hapo kwani kwa sasa shule hiyo ina mwalimu mmoja tu wa jinsia hiyo hali inayowakatisha tamaa wanafunzi wa kike kujiunga na masomo hayo.

Mwanafunzi Happiness Isack, kutoka shule hiyo ameiomba Serikali kuongeza walimu wa sayansi na hisabati, vitabu na kuboreshea miundombinu ya maabara ikiwemo vifaa vya kupimia kemikali.

Ziara ya wahandisi hao katika shule mbalimbali za Sekondari za mkoa huo inalenga kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa watoto wa kike ambapo leo shule zaidi ya Tano ikiwemo shule ya Mtama, Mahiwa, Ruangwa, Mbekenyera na Chinongwe zimeweza kufikiwa na huduma hiyo.