News

UJENZI WA JENGO LA ABIRIA MKOANI TABORA KUANZA KUJENGWA HIVI KARIBUNI

Posted On: Friday 30, November 2018

Imeelezwa kuwa ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora ambao utaweza kuchukua abiria 500 kwa wakati mmoja utaanza hivi karibuni ili kuufanya uwanja huo kuwa na hadhi ya kupokea ndege kubwa nyingi.

Hayo yamesemwa mkoani humo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, mara baada ya kukagua uboreshaji wa uwanja huo kwa awamu ya pili, ambapo pamoja mambo mengine amesema kuwa tayari mkataba umeshasianiwa kati ya Mkandarasi na Wakala wa Barabara (TANROADS) na fidia kwa wananchi zimeshalipwa.

"Jengo hili lililopo ni dogo ambalo linauwezo wa kubeba abiria 60 tu kwa wakati mmoja hivyo Serikali imeamua kuongeza ukubwa wa jengo hili ili liweze kuwa na hadhi ya kupokea abiria wengi kwa wakati mmoja", amesema Katibu Mkuu huyo.

Amefafanua kuwa ujenzi wa jengo hilo unagharamiwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 29.

Ameongeza kuwaujenzi wa jengo hilo mkoani humo utaenda sambamba na utekelezaji wa uboreshaji wa viwanja vya ndege vingine vitatu kwa kiwango cha lami ambavyo ni Kigoma, Sumbawanga na Shinyanga.

Mhandisi Nyamhanga amesisitiza juu ya lengo la uboreshaji wa viwanja vya ndege hapa nchini ambayo ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia usafiri wa Anga.

"Serikali inanunua ndege zenye ukubwa wa aina tofauti tofauti hivyo ni lazima ziende sanjari na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya viwanja vya ndege hapa nchini", amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Mapema Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, Godfrey Kaaya, alitoa taarifa kwa Katibu Mkuu huyo ya mradi wa upanuzi na uboreshaji wa kiwanja hicho kwa awamu ya pili uliohusisha upanuzi wa ujenzi wa maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami, barabara unganishi za kutua ndege ndogo, ujenzi wa mitambo ya kuongozea ndege, taa za kuongozea ndege, jengo la kuchukulia umeme na jeneta kubwa.

Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Nyamhanga, yupo katika ziara ya kikazi mkoani Taboraikiwa ni lengo la kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na sekta yake hususani barabara, madaraja na kiwanja cha ndege.