News

UJENZI WA DARAJA KATIKA ZIWA VICTORIA KUANZA MWAKANI

Posted On: Friday 23, November 2018

Naibu Waziri wa Ujenzi MheshimiwaElias John Kwandikwaamewataka wakazi wa mikoa ya Mwanza na Geita kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zitakazojitokeza wakati wa ujenzi wa daraja litakalounganisha eneo la Kigongo na Busisi Mkoani Mwanza.

Amesema maandalizi kwaajili ya ujenzi wa daraja hilo la aina yake hapa nchini yako katika hatua ya usanifu wa kina hivyo ujenzi wake utaanza mara baada ya mkandarasi wake kutangazwa nalinatarajiwa kuwa na urefu wa kilomita 3.2, litakapokamilika.

“Hakikisheni mnatoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi ya ujenzi iwe nyepesi na wale watakaopata fursa za ajira fanyeni kazi kwa weledi, bidii na nidhamu” amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ya muda mrefu hivyo ni jukumu la wananchi kujiandaa na kubaini fursa za kiuchumi na kijamii na kuzitumia.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya amesema daraja hilo litakuwa na njia nneza kupitisha magari, njia ya waenda kwa miguu ambapo pia litakuwa na kina kitakachoruhusu meli kupita chini ya daraja hilo.

Mhandisi Rubirya amesisitiza umuhimu wa wananchi wenye maeneo yatakayotumika kupisha ujenzi huo kutoa ushirikiano ili kuharakisha kazi hiyo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua kivuko cha Kigongo-Busisi na kuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi kuhusu usalama na matumizi sahihi ya utumiaji wa vivuko.

Amezungumzia umuhimu wa TEMESA kuweka mifumo ya kielektroniki ili kuwezesha waendesha vivuko, wakusanya mapato na wasimamizi kuwa na mawasiliano ya pamoja na hivyo kuwezesha vivuko kuwa na abiria na mizigo inayokubalika wakati wote.

Mkuu wa kivuko cha Kigongo –Busisi Mhandisi Abdala Atiki amesema kivuko hicho kwa sasa kinahudumiwa na Mv- Mwanza na Mv- Misungwi ambapo zaidi ya abiria elfu sita na mia tano huvushwa kwa siku.

Zaidi ya mikoa 12 nchini ina maeneo yenye mahitaji ya vivuko ambapo takriban vivuko 30 vinatoa huduma nchini kote.