News

SHIRIKIANENI BARABARA ZIKAMILIKE KWA WAKATI-KWANDIKWA

Posted On: Monday 06, August 2018

Imeelezwa kuwa ushirikishwaji, ushirikiano na uzalendo baina ya wadau wote wa ujenzi wa barabara nchini utawezesha unafuu wa gharama za ujenzi na ubora wa barabara zinazojengwa kukamilika kwa wakati.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa amesema hayo Wilayani Siha, Mkoani Kilimanjaro alipokagua ujenzi wa barabara ya Sanya Juu-Kamwanga Kilomita 74 na kusisitiza kuwa ni wakati sasa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), wananchi na Mkandarasi kufanya kazi pamoja ili kuwezesha tija na ufanisi kufikiwa kwa haraka katika mradi huo.

“Wananchi wa Wilaya za Siha, Longido na Rombo nawaomba mtoe ushirikiano kwa TANROADS na Mkandarasi ili kuwezesha kupatikana kwa urahisi wa kokoto, mchanga na nguvu kazi ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa wakati” amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Barabara ya Sanya Juu-Kamwanga ni sehemu ya barabara ya Boma Ng’ombe hadi Kamwanga yenye urefu wa KM 98 ambapo ujenzi wake umegawanywa katika sehemu tatu ambazo ni SanyaJuu- Elerai KM 32.2, Elerai-Kamwanga KM 42 na Bomang’ombe-Sanya Juu KM 24.

“Kukamilika kwa barabara hii kutachochea kasi ya uzalishaji katika mashamba, kutoa fursa mpya za ajira na kuongeza kasi ya utalii katika eneo la Mkoa wa Kilimanjaro” amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoani Kilimanjaro, Mhandisi Nkolante Ntije amesema zaidi ya shilingi bilioni 52 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza inayohusisha madaraja makubwa mawili, makalvati ya kati 110 na makalvati madogo 32 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika februari mwakani.

Mkandarasi anayejenga barabara hiyo China Geo-Engineering Corporation kutoka China , Bw Wang Tuquan amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa licha ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha juu cha ubora itamalizika kwa wakati.

Naibu Waziri Kwandikwa yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika Mkoani Kilimanjaro.