News

SERIKALI YAUNDA TUME KUBAINI CHANZO CHA MOTO JNIA

Posted On: Friday 13, January 2017

Serikali imesema imeunda Tume ya uchunguzi ya watu 12 ili kuweza kuchunguza na kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyotokea jana saa Tano usiku katika chumba kidogo cha kuhifadhia mizigo kilichopo kwenye jengo la Pili la abiria (Terminal II) katika uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwaTume hiyo iliyoundwa inaongozwana Joseph Nyahende ambae anatoka katika ofisi zaMakao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini.

“Ninategemea kupata ripoti ya kitaalamu kutoka kwa Tume hii, ili kutusaidia kubaini kiundani juu ya chanzo haswa kilichopelekea moto huu”, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua kuwa huduma katika jengo hilozinaendelea kama kawaida ambapo awali zilisitishwa na kuhamishiwa katika Jengo la Kwanza la abiria (Terminal I).

“Mara baada ya moto kutokea, kitu cha kwanza kilichofanyika ni kuudhibiti moto huu ili usiweze kusambaa katika maeneo ambayo hayajaathirika, kisha tukatafuta njia za kurudisha huduma kwa abairia”, amesisitiza Profesa Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa ameipa miezi miwilikampuni ya mizigo ya Swissport kurekebisha huduma zinazolalamikiwa na wateja wake na endapo itashindwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa JNIA, Paul Rwegasha ameeleza kuwa tathmini na gharama za mizigo iliyokuwa imehifadhiwa katika chumba hicho bado haijajukana, ambapo ripoti itaeleza gharama hizo pindi itakapokamilisha uchunguzi wake.