News

SERIKALI KUTOTOA KAZI YA UJENZI WA BARABARA KWA MKANDARASI ASIYEKUWA NA UWEZO WA KIFEDHA

Posted On: Saturday 01, September 2018

Serikali imeeleza kuwa haitatoa kazi za ujenzi wa miundombinu ya barabara hapa nchini kwa kampuni za ujenzi ambazo hazina uwezo wa kifedha wa kufanya kazi hizo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Kamwelwe, amesema hayo Wilayani Bunda, Mkoani Mara mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 na kubaini kuwa kampuni ya ujenzi ya Nyanza Road Works kuwa na uwezo mdogo wa kifedha na hivyo kuchelewesha mradi huo.

Mhandisi Kamwelwe ameeleza changamoto nyingine iliyochelewesha mradi ni kutokana na kampuni ya Inter Consult iliyofanya usanifu wa barabara kukosea michoro ya mradi huo na hivyo kumsababishia mkandarasi kushindwa kufanya kazi yake kikamilifu.

"Aliyesanifu mradi huu hakufanya vizuri na hivyo kumsababishia mkandarasi kuongezewa muda wa kazi miezi 35 mingine kutokana na kuongezeka kwa makalvati katika barabara hiyo na ukubwa wa tuta la barabara", alifafanua Waziri Mhandisi Kamwelwe.

Waziri huyo amemtaka Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya DOCH na Mkandarasi kuongeza vifaa na wataalam wengine ili kuhakikisha kasi ya mradi huo inaenda kwa haraka.

Aidha, Mhandisi Kamwelwe, ameiagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mara kumsimamia mkandarasi huyo ili akamilishe mradi huo ifikapo mwezi Juni mwakani badala ya mwezi Desemba 2019.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS, mkoa wa Mara Mhandisi Mlima Ngaile, amemuahidi Waziri Kamwelwe kuwa atamsimamia mkandarasi huyo kikamilifu na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango.

Katika hatua nyingine Waziri Mhandisi Kamwelwe amekagua ujenzi wa barabara ya Makutano - Sanzate yenye urefu wa KM 50 na kuridhishwa na kasi ya makandarasi 10 wazawa walioungana kupitia kampuni ya M/S Mbutu JV na kuwaahidi kuwaongeza sehemu ya barabara kutoka Sanzate hadi Nata na ile ya Mugumu hadi Serengeti pindi watakapokamilisha mradi huo.

Waziri Kamwelwe ameongeza kuwa pamoja na mradi wa barabara hiyo kuwa na maeneo korofi na mawe hadi sasa mradi umefikia asilimia 69 na KM 10 tayari zimeshawekwa lami.

Naye Mkandarasi wa Kampuni hiyo Mhandisi Andrew Nantori ameishukuru Serikali kwa kuwaamini makandarasi wazawa na amemuahidi Waziri Kamwelwe kuwa hatowaangusha.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Bulamba-Kisorya yenye urefu wa KM 51 na barabara ya Makutano-Sanzate yenye urefu wa KM 50 inafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.