News

SERIKALI KUONGEZA FURSA ZA WAHANDISI

Posted On: Friday 08, September 2017

Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi, amesema Serikali inafanya jitihada za kipekee kuongeza idadi ya wahandisi nchini ili kuiwezesha nchi kuwa na rasilimali watu ya kutosha katika fani ya Uhandisi, Sayansi, Hisabati na Teknolojia na hivyo kuharakisha ujenzi, ustawi, maendeleo ya viwanda na miundombinu.

Akizungumza katika madhimisho ya 15 ya Wahandisi yaliyoanza leo mjini Dodoma, Mhandisi Balozi Kijazi ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi Nchini (ERB), kuhakikisha wahandisi wanaoongezeka wanakuwa na viwango vya kutosha vya kitaaluma, kiujuzi na maadili ili kuleta matokeo chanya ndani na nje ya nchi.

"Serikali itahakikisha inafanya kila namna kuongeza nguvu kazi ya kutosha hasakatika kipindi hiki cha kujenga uchumi wa viwanda ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto za miundombinu, kiuchumi na kijamii", amesema Mhandisi Balozi Kijazi.

Ameongeza kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya mafundi sanifu kwenye uendelezaji wa viwanda, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), itatenga fedha kwa ajili ya kusomesha wataalamu hao kwa kiwango cha Stahahada (Diploma), katika vyuo mbalimbali nchini ili kupunguza uwiano baina ya wahandisi, mafundi sanifu na mafundi mchundo.

Aidha, ameipongeza Bodi hiyo kwa kusimamia utoaji wa mafunzo ya kuendeleza taaluma ya kihandisi yenye lengo la kuhakikisha wahandisi wanaendana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa Sekta ya Ujenzi itahakikisha taaluma ya uhandisi inakua kwa kuwaendeleza wahandisi kielimu na kimitaji ili waweze kujenga uchumi imara wa nchi na kuharakisha maendeleo.

Ameongeza kuwa Wahandisi wanaunga mkono nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufikia uchumi wa kati kwa kupitia viwanda ili kukidhi matarajio ya wananchi katika nyanja mbalimbali ifikapo 2025.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ERB Mhandisi Prof. Ninatubu Lema, amemhakikishia Katibu Mkuu Kiongozi kuwa wahandisi wataendelea kufanya kazi zao kwa weledi, nidhamu na kuzingatia maadili yao ya kazi kama wanavyoapa kufanya hivyo.

Amemuomba Katibu Mkuu Kiongozi, kuboresha mazingira ya Wahandisi nchini kwa kuwapa miradi mikubwa ya ujenzi wahandisi wazalendo ili kuwajengea uwezo wa ujenzi na usimamizi wake.

Zaidi ya wahandisi 2000 wameshiriki katika maadhimisho hayo ya 15 ya wahandisi yenye kauli mbiu "Jukumu la Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati katika Kukuza Viwanda kwa Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi", ambapowahandisi 150 wamekula kiapo cha utii na uaminifu.