News

SEKTA YA BARABARA YATAKIWA KUUWIANA NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Posted On: Wednesday 11, April 2018

Imeelezwa kuwa mafanikio endelevu katika sekta ya barabara na uchukuzi hapa nchini yatafikiwa endapo mkakati wa muda mrefu unaohitaji juhudi za pamoja za wadau wote utatekelezwa kikamilifu.

Mkakati huo ni kuwawezesha wadau wote katika jamii kuelewa umuhimu wa barabara na kuhakikisha mazingira yanayozunguka barabara hizo yanalindwa na kutuzwa na kila mmoja katika nyanja yake.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi msaidizi wa idara ya Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Melania Sangue wakati akifungua mafunzo ya tathimini na usimamizi wa mazingira kwa mafundi sanifu wa barabara, mafunzo yanayoendelea mjini Morogoro.

Mhandisi Sangeu amewataka mafundi hao kutoa elimu wanayoipata kwa wadau wote wa barabara ili kuwezesha ujenzi na usimamizi wa barabara kuzingatia kanuni za mazingira na maendeleo endelevu.

“Hakikisheni miradi yote ya barabara inafanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira Enviromental Impact Assesment EIA,ili iwe endelevu na isiyo changia madhara kwa jamii,”alisisitiza mhandisi huyo.

Aidha pamoja na maagizo hayo amewataka wataalamu hao wa ujenzi kusimamia ujenzi wa barabara na hifadhi za barabara kwa kudhibiti uchimbaji wa mawe na mchanga kandokando ya barabarahali inayochangia uharibifu wa barabara kwa muda mfupi pindi ujenzi unapokamilika.

Kwa upande wake mdau wa mazingira Mhandisi Mary Assey amewataka mafundi hao sanifu kuhakikisha kuwa mafuriko,mmomonyoko wa udongo katika miradi ya ujenzi vinadhibitiwa wakati wote wa ujenzi na mara baada ya ujenzi huo kukamilika.

Mhandisi huyo amesema miradi mingi ya barabara inapokamilika wakandarasi wamekuwa wakiacha jamii zikiathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na athari za mazingira na kwamba kama wajenzi wa barabara hawatachukua hatua madhubuti za kudhibiti maeneo walikofanya uchimbaji mchanga athari zitakuwa endelevu.

Naye mtaalamu wa ujenzi Mhadisi Chacha Harun kutoka wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano amesema kwa sasa wamejipanga kuhakikisha uharibifu wa mazingira unaosababishwa na miradi ya ujenzi wa barabara unadhibitiwa na miradi hiyo kuwa endelevu kwa jamii husika.

Mafunzo hayo yametolewa kwa wahandisi 425 na mafundi sanifu 466 kutoka miko yote ya Tanzania bara ikiwa ni mkakakati wa kuhakikisha ujenzi wa barabara unakwenda sambamba na usimamizi wa usalama wa mazingira katika miradi yote nchini.