News

RAIS DKT. MAGUFULI ATOA SIKU 5 MKANDARASI ALIPWE FEDHA ZA AWALI

Posted On: Wednesday 03, April 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ametoa muda wa siku 5 kwa Mawaziri wawili ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Waziri wa Fedha na Mipango kuhakikisha wanampatia malipo ya awali ya asilimia 15 mkandarasi anayejenga Kiwanja cha Ndege cha Mtwara.

Amesema hayo mkoani Mtwara kabla ya kuweka jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho ambapo moja ya sababu zilizochelewesha mradi kuanza ilikuwa ni malipo ya shilingi bilioni 7.5.

"Naagiza Mawaziri mzungumze na ndani ya siku tano mkandarasi awe amelipwa", amesema Mhe. Dkt. Magufuli.

Mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho ulianza mwezi Juni mwaka 2018 na mkandarasi M/S Beijing Construction Engineering Group Company kwa gharama ya shilingi bilioni 50.4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2020.

Ametoa wito kwa Wizara, Mhandisi elekezi anayesimamia mradi huo kutoka kitengo cha kihandisi cha TANROADS (TECU) kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa haraka iwezekanavyo.

"Hakikisheni mnamsimamia vizuri mkandarasi huyu na anakamilisha mradi huu kwa wakati na akishindwa mfukuzeni", amesisitiza Dkt. Magufuli.

Amemtaka mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana baada ya kukamilishiwa malipo yake aliyokuwa anadai Serikali.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameeleza kuwa kiwanja cha Ndege cha Mtwara ni miongoni mwa viwanja vya kimkakati kwa masuala ya ulinzi wa nchi yetu na ni kichocheo muhimu kwa biashara na usafiri wa kawaida wa abiria katika ukanda wa kusini na nchi jirani.

Amesema kwa sasa kiwanja hiki ni chadarajala 3C na kina idadi ya miruko (flights) ya ndege inayofikia 1,000 kwa mwaka inayojumuisha ndege zote ndogo na kubwa aina ya Bombardier Q-400, Boeing 737, ATR-72 na kinahudumia abiria wapatao 35,000 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Crispianus Ako, amesema kuwa ukarabati na upanuzi utakapokamilika kiwanja kinategemewa kuhudumia hadi ndege za daraja 4E aina ya Airbus A330, Boeing 777 na Boeing B787-8.

Ameongeza kuwa idadi ya abiria inatarajiwa kuongezeka kutoka abiria 35,000 kwa sasa hadi abiria 500,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.

Ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho ni azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha inaboresha miundombinu chakavu iliyojengwa toka enzi za mkoloni mwaka 1952/53 na kuongezafursa za uwekezaji katika biashara, kilimo, gesi, madini, viwanda na utalii.