News

RAIS AAGIZA UPANUZI WA KIWANJA CHA NDEGE TABORA

Posted On: Wednesday 26, July 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza kupanuliwa kwa urefu wa kiwanja cha ndege chaTabora kutoka KM 1.9 zilizopo sasa hadi kufikia KM 2.5 ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa usafiri wa anga katika mkoa huo.

Akitoa agizo hilo katika ufunguzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho mkoani humo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, Rais Magufuli, amesema kuwa upanuzi wa kiwanja hicho utapelekea kuruhusu hata ndege kubwa za kutoka nje ya nchi kuweza kutua kiwanjani hapo.

"Mji wa Tabora ni mji unaokua kwa kasi sana, hivyo ni muhimu kwa Wizara kuona namna ya kuongeza uwanja huu ili kuwezesha ndege zote kuweza kutua, kwa sasa kiwanja hichi bado ni kidogo kwani hata ndege ya Rais hapa haiwezi kutua", amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli pia amemtaka Waziri huyo kuhakikisha anajenga jengo kubwa na la kisasa litakaloweza kuchukua abiria 500 kwa wakati mmoja kwani jengo lililopo sasa linachukua abiria 50 hali inayopelekea msongamano katika jengo hilo.

"Tumieni fedha za mkopo za Umoja wa Nchi za Ulaya ambazo wametupatia kwa ajili ya miradi ya maendeleo na ikiwezekana ujenzi wa jengo hili uanze mwaka huu", amesisitiza Rais Magufuli.

Amewataka wafanyakazi wa viwanja vya ndege nchini kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi na kutokuwa na utamaduni wa kupenda rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amefungua miradi miwili ya barabara mkoani humo ambayo ni barabara ya Tabora - Nyahua yenye urefu wa KM 85 na barabara ya Tabora - Puge - Nzega KM 114.9.

Kwa upande wake, Waziri Prof. Mbarawa, amemuahidi Rais Magufuli kutekeleza maagizo ya upanuzi wa urefu wa kiwanja hicho na ujenzi wa jengo la abiria haraka iwezekanavyo.

"Nakuahidi Mhe. Rais kufanyia kazi maagizo yako yote ulionipa, nitakaa na watendaji wangu kuona namna ya kuyatekeleza mapema iwezekanavyo", amesema Waziri Mbarawa.

Mradi huo ni moja ya jitihada za Serikali katika kufufua na kukarabati viwanja vya ndege nchini ili kuhakikisha inaboresha sekta ya anga.