News

PROF. MBARAWA AWATAKA WATENDAJI KUTUMIA HEKIMA KUONGOZA.

Posted On: Thursday 08, March 2018

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa, Makame Mbarawa amewataka watendaji kutumia hekima katika kuongoza ili kuwezesha wafanyakazi waliochini yao kufanyakazi kwa weledi, ubunifu na hivyo kuzibadili changamoto zinazowakabili kuwa fursa.

Akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), mjini Dodoma Profesa, Mbarawa amewataka watendaji na wafanyakazi kujitathmini kila wakati ili kazi wanazofanya ziwe na matokeo chanya na yanayopimika kwa haraka.

“Wafanyakazi ndio nguzo ya mafanikio popote mahali pa kazi hivyo ni vema kila kiongozi akafamu na kuamini hivyo kwa manufaa ya taasisi anayoiongoza”, amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Profesa, Mbarawa ameipongeza TMA kwa kupata cheti cha ubora wa viwango ISO-9001:2015 katika utoaji wa huduma ya upimaji wa hali ya hewa katika usafiri wa anga na majini na kuifanya TMA kutambulika kimataifa.

“Hongereni kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu mbele ya Nigeria na Afrika Kusini katika ubora wa utabiri na hivyo tumieni ubora huu kuongeza mapato na kutoa elimu kwa wananchi wengi zaidi”, amesisitiza Prof, Mbarawa.

Amewataka wafanyakazi kukumbuka kuwa kujenga imani ni jambo kubwa ila kuiondoa imani ni jambo la dakika moja, hivyo popote wanapoaminiwa wailinde imani hiyo.

Naye Mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agness Kijazi amemhakikishia Prof. Mbarawa na watanzania kuwa wamejipanga kuhakikisha utabiri wao unaendelea kuwa wa uhakika na kuongeza vituo vya hali ya hewa ili jamii kubwa hapa nchini inufaike kiuchumi na kijamii na utabiri wao.

Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA pamoja na kutathmini mafanikio na changamoto za utendaji kazi wa Mamlaka hiyo pia kitapitisha bajeti ya mamlaka hiyo ya mwaka wa fedha 2018/2019.