News

PROF. MBARAWA: ATOA TAHADHARI UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU

Posted On: Monday 19, December 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewatahadharisha watanzania kuepuka vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya barabara husasan katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Ameyasema hayo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma-Babati yenye urefu wa KM 188.1, sehemu ya Mela-bonga ambapo imeripotiwa kuwepo vitendo vya uharibifu wa miundombinu kwa muda mrefu.

'Napenda kutoa wito kwa watanzania kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuacha vitendo vya kuchoma matairi barabarani, kwani hali hii hupelekea kuharibu barabara kwa kiasi kikubwa ambazo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuzijenga", amesema Prof.Mbarawa.

Aidha, amekemea vitendo vya baadhi ya madereva kumwaga mafuta barabarani na baadhi ya wananchi kupitisha mifugo kwenye barabara ambapo vyote kwa pamoja vinaharibu miundombinu ya barabara.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali ikiwemo kuwaripoti wale wote wanaohujumu miundombinu ya barabara nchini.

Sambamba na hilo, amewaasa madereva wa vyombo vya moto kuwa makini barabarani kwa kuzingatia sheria za alama za barabara ikiwemo kuendesha vyombo hivyo kwa mwendo unaotakiwa ili kudhibiti ajali za barabarani zinazoweza kuepukika.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma- Babati yenye urefu wa KM 188.1, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa barabara hiyo inatarajiwa kukamilika mwakani kwani kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za ujenzi wake.

"Kazi inaenda kwa kasi kubwa, matumaini yangu ni kwamba ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017, barabara hii itakamilika kwa viwango bora tulivyokubaliana kwenye mkataba", amesisitiza Profesa Mbarawa.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza umbali wa masaa kwa abiria wanaosafiri kupitia njia ya Singida wanaotoka Dodoma na mikoa ya jirani kuelekea Manyara, Moshi na Arusha.

Ameongeza kuwa barabara hiyo itasaidia kuiunganisha Tanzania na Nchi za kutoka Kusini na Kaskazini mwa bara la Afrika, hivyo kufungua fursa za kibiashara kwa wananchi na kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa viwago vinavyostahili na kuahidi kukamilika kwa wakati.