News

PROF. MBARAWA APEWA MWEZI MMOJA UJENZI WA BARABARA

Posted On: Sunday 23, July 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, kutangaza zabuni na mkandarasi kuanza na kumaliza kazi ya ujenzi wa barabara ya Kaliua - Urambo (km 28) kwa kiwango cha lami ndani ya mwezi mmoja.

Agizo hilo amelitoa leo mara baada ya kufungua barabara ya Kaliua- Kazilambwa (km 56) na barabara ya Urambo - Ndono - Tabora (km 94) zilizojengwa kwa kiwango cha lami ambapo amesisitiza kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kwa kutumia fedha za ndani na kumtaka Waziri pamoja na watendaji wake kulifanyia kazi agizo hilo.

"Pofesa Mbarawa hakikisha unatafuta mkandarasi wa kuijenga barabara hii na kuimaliza ndani ya mwezi mmoja, hakuna sababu ya mtu kupita tena katika njia ya vumbi iliyobaki kutoka Kaliua kwenda Urambo wakati fedha tunazo", amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri huyo kutafuta mkandarasi na kuanza kazi ya kujenga barabara ya Chaya - Nyahua (km 84) kwa kiwango cha lami ndani ya siku 45 ambapo amesema kuwa fedha za mradi huo zitatolewa na Mfuko wa Mfalme wa Kuwait (Kuwait Fund).

Kuhusu wananchi wanaovamia miundombinu ya reli na barabara Rais Magufuli, amewataka kujiandaa kisaikolojia kuvunjiwa nyumba zao kwani Serikali yake haitamvumilia yeyote anaevunja sheria hata kama ni kiongozi.

"Wananchi mliojenga katika hifadhi za reli na barabara sasa mjiandae, Mameneja mhakikishe kuwa mnasimamia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa yeyote anaevamia miundombinu hii", amesisitiza Rais Magufui.

Rais Magufuli amewataka madereva na wananchi kutunza miundombinu ya barabara nchini kwa kutozidisha mizigo yenye tani zaidi ya 56 kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007 kwani kufanya hivyo ni kuiharibu miundombinu hiyo ambapo Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa katika ujenzi wake.

Kwa upande wake, Waziri Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa mbalimbali na kuchochea maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani ya Katavi na Kigoma.

"Wananchi wa mkoa wa Tabora sasa ni jukumu lenu kuitunza na kuilinda barabara hii ambayo mmeisubiri kwa muda mrefu", amesema Profesa Mbarawa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusogeza karibu maendeleo kwa wananchi wake hususan ya barabara, maji, umeme, afya na elimu.

Mradi wa barabara ya Kaliua - Kazilambwa (km 56) umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 61.86 na ule wa Urambo - Ndono – Tabora (km 94) umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 118.96 ambazo zote ni fedha za ndani.