News

NAIBU WAZIRI KWANDIKWA AHIMIZA WAKANDARASI KUUNGANA

Posted On: Tuesday 07, August 2018

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa amezungumzia umuhimu wa wakandarasi wazawa kuungana ili waweze kupata miradi mingi ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini.

Akizungumza mara baada ya kukagua barabara ya Kikweni-Lomwe-Ndolwe-Kilomeni-Lembeli yenye urefu wa Kilomita 42.5 Naibu Waziri Kwandikwa amesema ni sera ya Serikali kuwawezesha wakandarasi wazawa hivyo ni jukumu lao kuungana ili kunufaika na fursa ya kupata miradi mingi.

“Unganeni ili tuwawezeshe mpate miradi mingi ndani na nje ya nchi ili muongeze fursa za ajira, mitaji, na kukuza uchumi wa nchi,” amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Akizungumza katika ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe ameiomba Serikali kuongeza ujenzi wa barabara za lami katika tarafa za Ugweno na Usangi ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kukuza biashara katika Wilaya hiyo na kuwezesha mazao mengi ya milimani kufika maeneo ya mjini kwa urahisi.

Aidha, amempongeza Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Nkolante Ntije kwa kuhakikisha barabara za Wilaya ya Mwanga zinapitika wakati wote wa mwaka.

Barabara ya Kikweni hadi Lomwe yenye urefu wa Kilomita 10.9 inajengwa kwa ushirikiano wa Kampuni za Kizalendo za Bona & Hurbert Engineering na Builders & Lime Works ambapo hadi sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia zaidi ya sitini.

Naibu Waziri Kwandikwa yuko katika ziara ya siku tatu kukagua maendeleo ya ujenzi wamiundombinu katika Mkoani Kilimanjaro.