News

NAIBU WAZIRI KWANDIKWA AFUATILIA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA RAIS

Posted On: Sunday 08, December 2019

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa amewataka viongozi wote wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita kushirikiana na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), kuhakikisha ujenzi wa barabara za lami katika mji wa Masumbwe unakamilika kwa wakati.

Amesema uwepo wa barabara nyingi za lami katika wilaya za Mbogwe na Kahama utachochea fursa nyingi za utalii, ufugaji, uchimbaji madini na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na hivyo kukuza uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA wilayani humo mhe. Kwandikwa amesema atahakikisha ujenzi wa kilomita zote tatu zilizoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Joseph Magufuli unakamilika kama ilivyopangwa.

Hakikisheni mnawaelimisha wananchi ili wapishe maeneo yote zitakapopita barabara hizo ili kusiwe na vikwazo kwa wajenzi wa barabara hizo”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Hivi karibuni katika ziara yake wilayani humo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Joseph Magufuli aliagiza utekelezwaji wa haraka wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa tatu alizoahidi katika makao makuu ya wilaya ya Mbogwe na kusisitiza kazi hiyo ifanyike haraka.

Naye mkuu wa wilaya ya Mbogwe Bi, Martha John Mkupasi amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa ushirikiano wakati wa ujenzi wa barabara hizo na kuzilinda pindi zitakapokamilika ili kuboresha miundombinu ya wilaya hiyo na kukuza shughuli za biashara.

Amehimiza wananchi kutovamia maeneo ya hifadhi ya barabara ili kuepuka usumbufu wakati zoezi la ujenzi linapoendelea.

Kwa upande wake meneja wa TARURA wilayani humo Eng. Justine Lukanga ameahidi ujenzi wa kilometa tatu za lami katika barabara ya Mashineni-Kasandalala km 1.3 na Mang’ombe-Iloganzala 1.2 na kituo cha afya-shuleni km 0.5 zitajengwa kwa kasi na ubora unaozingatia thamani ya fedha.