News

MHANDISI NYAMHANGA: HAKUNA SABABU ZA KUCHELEWESHA MRADI

Posted On: Friday 30, November 2018

Serikali imewataka Makandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa KM 359 inayounganisha Mkoa wa Tabora na Katavi kupitia daraja la Koga, kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha mradi huo kabla ya muda uliopangwa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph nyamhanga, wakati wa ziara yake katika mikoa hiyo ambapo amesema fedha za mradi huo zipo hivyo hakuna sababu ya kuuchelewesha.

"Fedha za ujenzi wa mradi huu zipo hivyo fanyeni kazi usiku na mchana ili kukamilisha mapema barabara hii kwani hakuna vikwazo vyovyote na mvua isiwe sababu ya kusimamisha kazi za ujenzi", amesema Mhandisi Nyamhanga.

Mhandisi Nyamhanga, amewataka wasimamizi wa mradi wakishirikiana na Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mikoa hiyo kusimamia mradi huo kwa ukamilifu na kwa ubora uliopangwa bila kuongeza gharama.

"Hakikisheni mradi huu unasimamiwa kwa ubora uliopangwa na mdhibiti gharama za mradi hata ikiwezekana ipatikane akiba ya fedha ambayo itatumika kwa miradi mingine ya barabara hapa nchini", amesisitiza Katibu Mkuu huyo.

Ameeleza umuhimu wa kukamilika kwa barabara hiyo kuwa utakuza uchumi wa wananchi na kuongezeka kwa shughuli za kibiashara kwakuwa ni miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji mwingi wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji wa nyuki, madini na utalii.

Kuhusu uharibifu wa miundombinu ya barabara hapa nchini, Mhandisi Nyamhanga, ametoa wito kwa wananchi wa mikoa hiyo kuilinda miundombinu hiyo kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekamatwa.

Aidha, amewataka wananchi ambao wanaguswa na miradi inayoendelea kuhakikisha kwamba hakuna wizi wa vifaa vya ujenzi, nondo, uharibifu wa mitambo ya makandarasi, mafuta na saruji kwani kunarudisha nyuma utekelezaji wa miradi hiyo nakuongeza gharama.

Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Nzaga, Bw. Karoli Kilanga, ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani kutapunguza gharama za usafiri na kupunguza muda waliokuwa wakipoteza hasa vipindi vya mvua magari mengi yalikuwa yanakwama kutokana na ubovu wa barabara.

Mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda unajengwa kwa sehemu tatu ambazo ni kutoka Usesula - Komanga, sehemu ya Komanga-Kasinde na sehemu ya Kasinde-Mpanda ambapo utagharimu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 481 na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2021.