News

MELI ZA MV RUVUMA NA NJOMBE KUANZA KAZI JANUARI

Posted On: Monday 21, November 2016

Imeelezwa kuwa uchumi wa wananchi wa Mikoa ya Njombe, Mbeya na Ruvuma utaimarika kwa kasi kama watatumia vizuri fursa ya uwepo wa meli za mizigo na abiria katika ziwa Nyasa.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kukamilika kwa meli mbili za mizigo za Mv. Njombe na Mv. Ruvuma na ujenzi wa meli ya abiria ya Mv. Mbeya ni fursa mpya ya kiuchumi kwa wakazi wa mikoa hiyo.

“Tumejipanga kuhakikisha tunafungua ukanda huu wa nyanda za juu kusini kiuchumi hivyo ni jukumu la wananchi kuchangamkia fursa za kibiashara zinazoweza kusafirishwa ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi”.amesema Eng. Ngonyani.

Naibu Waziri Ngonyani ameelezea kuridhishwa kwake na hatua ya ujenzi wa meli za Mv.Njombe na Ruvuma ambao umefikia asilimia tisini na tisa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaamini makandarasi wazawa wanaofanya kazi kwa ubunifu, uadilifu na uaminifu ili kutoa fursa nyingi za ajira kwa watanzania.

Kaimu Meneja wa bandari ya Itungi na Kiwira Eng. Juma Kisavara amemhakikishia Naibu Waziri Ngonyani kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imejipanga kuhaikikisha bandari zote kumi na tano zilizopo katika ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania zinafufuliwa na kutumika kupakia na kushusha mizigi ikiwemo vifaa vya ujenzi, makaa ya mawe,mbolea na mazao ambayo yana soko ndani na nchi za jirani.

Eng. Kisavara amemhakishia Naibu wa Ujenzi kuwa tayari wametafuta soko la kutosha la kusafirisha mizigo hivyo kuiomba Serikali kuendelea na kasi ya ujenzi wa meli nyingine zitakazotumika katika ziwa Nyasa.

Zaidi ya shilingi bilioni 11 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa Meli ya Mv.Ruvuma na Mv. Njombe zinazojengwa na kampuni ya Songoro Marine Transport ya hapa nchini na meli hizo zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali mwezi Januari mwakani.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ngonyani amekagua ujenzi wa barabara ya Kikusya-Ipinda hadi Matema KM 34.6 wilayani Kyela inayojengwa kwa kiwango cha lami na kusisitiza kuwa Serikali italipa fedha kwa mkandarasi anayejenga barabara hiyo ili kuiwezesha kukamilika kwa muda uliopangwa.