News

MBARAWA AAGIZA TAASISI NCHINI KUJIUNGA NA KITUO CHA KUMBUKUMBU (IDC)

Posted On: Tuesday 17, January 2017

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameziagiza Taasisi zote za Serikali nchini kuhakikisha zinaleta taarifa zao kuhifadhiwa katika kituo cha Taifa cha Kuhifadhi kumbukumbu cha Kijitonyama (IDC) kwani kituo hicho ni salama na kina ubora wa hali ya juu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Aidha, amezitahadharisha baadhi ya Taasisi zenye mpango wa kujenga nakuanzisha vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu kuacha mara moja mpango huo, kwani kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya kituo hicho na kupoteza fedha za Serikali.

Hayo yamezungumzwa jijini Dar es salaam na Waziri huyo mara baada yakutembelea kituoni hapo na kupokea taarifa ya uendeshaji wa kituo hicho kutoka kwa Mkuu wa Kituo, Abdul Mombokaleo.

“Sioni sababu kwa Taasisi nyingine kutaka kujenga vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu, Serikali imeshawekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki, hivyo taasisi zote nchini zinalazimika kutumia kituo hiki”, amesema Profesa Mbarawa.

Sambamba na hilo amezisisitiza kampuni zilizo chini ya Wizara yake kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine nchini kwa kuwa wa kwanza kuleta taarifa zao kuhifadhiwa katika kituo hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo hicho Abdul Mombokaleo, amefanunua kuwa hadi sasa wameshafanikiwa kuunganisha wateja 13 kujiunga na kituo hicho na wengine zaidi ya 40 wapo katika mchakato wa kujiunga.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea ofisi za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kusema kuwa ameridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo kutokana na jitihada zake za kuteka soko la ushindani katika makampuni ya mawasiliano nchini.

“Nimefarijika zaidi kuona sasa TTCL inafanya vizuri katika eneo la masoko kwani nimeshuhudia matangazo mengi barabarani, kwenye luninga, magazetini na katika mitandao ya kijamii, hii inadhihirisha sasa mna mpango wa kuifufua kampuni hii”, amefafanua Profesa Mbarawa.

Ameutaka uongozi wa kampuni hiyo kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa uadilifu na ushirikiano ili kuleta mabadiliko chanya yatakayoboresha kampuni hiyo na kuteka zaidi soko la mawasiliano nchini.