News

KWANDIKWA: BARABARA ZA MCHEPUO KUPUNGUZA MSONGAMANO DODOMA

Posted On: Saturday 20, January 2018

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Mbande - Kongwa (Km 11.7) na Chimwaga - Ihumwa (Km 10) utasaidia kupunguza msongamano kwa magari yanayoingia Dodoma mjini.

Naibu Waziri huyo ameyasema hayo wakati akikagua barabara hizo na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambapo amesisitiza kwa makandarasi wanaojenga barabara hizo kuhakikisha wanamaliza kazi hizo kwa muda uliopangwa na kwa viwango vilivyo kwenye mkataba.

"Tutaendelea kujenga na kuboresha barabara hizi za mchepuo lengo ni kupunguza foleni katikati ya mji kwani Dodoma sasa inakua kutokana na uwepo wa watumishi wengi wa Serikali na ongezeko la magari, kwa hiyo sisi kama Serikali hatuna budi kuangalia namna ya kuboresha miundombinu yetu ili ikidhi haja ya ongezeko hili", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, amefafanua kuwa barabara hizo zikikamilika zitakuwa ni njia mbadala kwa watumiaji kwani sio lazima kwa magari yote kupita mjini na badala yake yatatumia njia nyingine za mchepuo kuendelea na safari zake.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua athari za mvua katika barabara za mji wa Dodoma na kuwataka wananchi na madereva kuchukua tahadhari ili kuepusha hatari zinazoweza kuwakabili wakati wakivuka ama kupitisha magari yao katika kipindi hiki ambacho baadhi ya sehemu za barabara zinajaa maji kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha.

Amewaomba viongozi mbalimbali wa Serikali kushirikiana katika kutoa ushauri kwa wananchi kuhusu utafutaji wa maeneo yanayowafaa kuishi ili kunusuru maisha yao na mafuriko ambayo yanaweza kuwakabili kutokana na kuchagua maeneo yasiyo sahihi kwa makazi ya binadamu.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, amefafanua kuwa barabara ya Mbande- Kongwa yenye urefu wa KM 11.7, kwa sasa imejengwa kilometa Tano ikiwa ni awamu ya kwanza na kufikia mwezi ujao watajenga tena kilometa nyingine Tano.

Naye, Msimamizi wa ujenzi wa barabara ya Chimwaga - Ihumwa yenye urefu wa KM 10 kwa kiwango cha lami, Mhandisi Nicholaus Mzeru, amesema mradi ulianza mwaka 2013, ambapo kwa sasa umefika asilimia 92.4 na kilometa 8 tayari zimeshajengwa.

Ujenzi wa Barabara ya Chimwaga- Ihumwa (Km 10), inajengwa na mkandarasi Nyanza Road Works kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 15 ambapo ujenzi wake unaendelea na unategemewa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.