News

KIWANJA CHA NDEGE CHA ZIWA MANYARA KUKARABATIWA

Posted On: Sunday 05, August 2018

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa Serikali iko kwenye hatua za awali za kukarabati kiwanja cha ndege cha Ziwa Manyara kutokana na umuhimu wake katika shughuli za utalii kwenye mbuga za Manyara na Ngorongoro.

Akizungumza katika ziara hiyo mkoani Arusha Waziri Kamwelwe, amefafanua kuwa Kiwanja hicho ni miongoni mwa viwanja 11 vilivyo katika mpango wa kufanyiwa ukarabati na Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na hivyo kusisitiza kuwa kukamilika kwake kutaongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii.

"Serikali tumepata fedha ili kukiboresha kiwanja hiki na fedha hizo zitaelekezwa kwenye uimarishaji wa miundombinu ya barabara za kuruka na kutua ndege ili kuwezesha ndege ziweze kutua kwa urahisi", amesema Mhandisi Kamwelwe.

Aidha, ameongeza kuwa katika mikataba itakayosainiwa katika viwanja vya ndege miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ununuzi wa magari ya zimamoto kwa kuwa ni miongoni mwa changamoto katika viwanja vya ndege vingi.

Naye Meneja wa Kiwanja hicho Bw. Ezekiel Mwalutende, amemueleza Waziri huyo kuwa kiwanja hicho kinakusanya zaidi ya shilingi milioni 30 kwa mwezi kama tozo ya abiria na zaidi ya milioni 20 kama tozo kwa ndege zinazotua na kuruka.

Kuhusu changamoto za kiwanja Bw. Mwalutende, amemuelezea Waziri Mhandisi Kamwelwe, kuwa pamoja na changamoto nyingine kwenye kiwanja hicho pia kuna ukosefu wa taa kwenye maegesho ya ndege, uchakavu wa gari la zimamoto, uzio pamoja na uchavu wa njia za kuruka na kutua ndege.

Kiwanja cha Ndege cha Ziwa Manyara kina urefu wa mita 1220 na upana wa mita 23 na uwezo wa kuhudumia ndege zenye uzito wa tani saba na pia kina uwezo wa kuhudumia takriba ndege 42 kwa siku zenye uwezo wa kubeba abiria 18 kila ndege na maegesho ya ndege 6 kwa wakati mmoja.