News

KATIBU MKUU ATOA MIEZI 3 KWA KAMPUNI YA CHINA RAILWAY KUKAMILISHA MRADI

Posted On: Friday 30, November 2018

Serikali imetoa muda wa miezi mitatu kwa mkandarasi anayejenga kwa kiwango cha lami barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 kukamilisha ujenzi huo.

Agizo hilo limetolewa mkoani Rukwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo na kumtaka kuongeza kasi ya ujenzi huo.

"Hakikisheni mnaongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili muikabidhi barabara hii kwani imechukuwa muda mrefu", amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa na kampuni ya China Railway 15 group ni muhimu katika kuinua uchumi ya nchi yetu katika sekta ya usafirishaji wa mizigo kupitia bandari ya Kasanga kwani inaunganisha nchi yetu na nchi tatu ambazo ni Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia Ziwa Tanganyika

Ameongeza kuwa mkandarasi mpaka sasa ameshalipwa madeni yake ya nyuma na hivyo hana sababu ya kutokuikamilisha barabara hiyo.

Aidha, Mhandisi Nyamhanga amezitaja barabara ambazo zimekamilika ujenzi wake kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Sumbawanga-Tunduma KM 225, barabara ya Sumbawanga - Kibaoni KM 151 na barabara ya kutoka Sitalike hadi Sumbawanga Mjini KM 36.5

Amesema kuwa katika kuhakikisha nchi yetu inaungana na nchi jirani, Serikali inaendeelea kutafuta fedha kwa ajili ya barabara ya Matai hadi Kashesa yenye urefu wa KM 50 inayatuunganisha na nchi ya Zambia

Naye Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS), Mhandisi Masuka Mkina, amesema mradi huo unagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 133 na mpaka sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 80.

Mhandisi Mkina amefafanua kuwa mradi huo umehusisha ujenzi wa daraja kubwa la Kalambo lenye urefu wa mita 84 ambapo limekamilika na KM 75 za barabara hiyo tayari zimeshawekwa lami na kazi zingine zinaendelea.

Katika hatua nyingine Mhandisi Nyamhanga amekagua Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ambapo Serikali imeshakamilisha maandalizi ya kuanza uboreshwaji wa kiwanja hicho na tayari mkataba umeshasainiwa kati ya mkandarasi na Tanroads.

Ameagiza makampuni ya simu yaliyojenga minara iliyopo karibu na uwanja huo kuondoa haraka ili kutokwamisha mradi huo kukamilika mapema.

Amesema kuwa Serikali imetoa bilion 3.7 kwa ajili ya fidia na wananchi wameonesha ushirikiano kwa kubomoa majengo yao hivyo ujenzi hauna vikwazo vyovyote.

Amefafanua kuwa uboreshwaji huo katika kiwanja hicho utahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami, ujenzi wa njia za maungio, ujenzi wa maenegesho ya ndege, jengo la kisasa la abiria, ujenzi wa jengo la kuongozea ndege, ujenzi wa kituo cha hali ya hewa na usimikaji wa taa za kuongozea ndege.