News

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAIPA TANO TBA

Posted On: Tuesday 17, March 2020

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ubunifu ilioufanya wa kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali na kununua mitambo mbalimbali ili kupunguza gharama za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota.

Mradi huo ambao ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli mwaka 2016 alipowatembelea wakazi

wa Magomeni na kuwaahidi kuwajengea nyumba za kisasa.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, amewasisitiza TBA kutumia vizuri sehemu ya eneo lililobaki kwa kujenga majengo na nyumba za biashara ili kuongeza kipato.

“Kama kamati nawapongeza sana kwa kujenga nyumba hizi nzuri kwa wananchi wa kipato cha chini ni imani yangu kuwa kukamilika kwake kutapunguza changamoto ya makazi kwa wakazi waliohamishwa katika eneo hili’

Kakoso ameongeza kuwa ni wakati sasa TBA irudishe taswira iliyokuwepo kwa washitiri wake kwani imefanya vizuri kwa miradi mikubwa inayotekelezwa jijini Dar es Salaam na hivyo kuongeza nguvu kwenye miradi ya mikoa na wilaya zote hapa nchini.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikw,a amemuahidi Mwenyekiti na Kamati kuwa Serikali itaendelea kuwa karibu na Wakala huo ili kuhakikisha unakamilisha miradi kwa viwango na kwa wakati na itaendelea kuijengea uwezo ili iweze kujitegemea.

“Nikuhakikshie Mwenyekiti sisi kama wizara tuko karibu sana na wakala huu na tutahakikisha unaendelea kutekeleza miradi kwa wakati hasa katika maeneo yanayosuasua’ amesisitiza Kwandikwa.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TBA, Mbunifu Majengo Daud Kondoro, amesema kuwa mradi huo ukikamilika unaweza kuchukua familia zaidi 100 na unatarajia kukamilika mwezi juni, 2020.

Ameongeza kuwa mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 70 na kazi zinazoendelea kwa sasa ni kupaka rangi kwenye majengo hayo, kuweka madirisha ya aluminium na kukamilisha ghorofa ya nane ambayo ndio ya mwisho kwa majengo hayo.

Mradi huu wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota unatekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali kwa asilimia mia moja na unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 30.