News

KAMATI YA KUDUMU YA MIUNDOMBINU YAIPONGEZA KADCO

Posted On: Monday 02, July 2018

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeupongeza uongozi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), kwa usimamizi na uendeshaji mzuri wa kiwanja hicho na kuwezesha kiwanja kuendelea kuwa daraja la tisa kimataifa.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya kiwanja hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Selemani Kakoso, amesema ongezeko la idadi ya watalii wanaoingia na kutoka kiwanjani hapo ni sababu ya usimamizi mzuri na kusisitiza kampuni hiyo kubuni utaratibu mzuri wa kuongeza idadi ya mizigo.

“Niwapongeze sana uongozi na watumishi wa KADCO kwa mabadiliko makubwa mliyoyafanya katika kiwanja hiki kwani kwa muda mfupi baada ya miundombinu kuboreshwa mumeweza kuongeza idadi ya ndege na kuongeza pato la kampuni” amesema Mhe. Kakoso.

Aidha, Mhe. Kakoso ameitaka Kampuni hiyo kuongeza fedha kwenye huduma ya jamii ili wananchi wanaozunguka kiwanja hicho waweze kunufaika.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu katika kiwanja hicho lazima uende sambamba na utoaji bora wa huduma ili watalii mbalimbali wanaoingia na kutoka nchini wafurahie huduma.

Kuhusu mgogoro wa wananchi wanaozunguka kiwanja hicho, Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dr Lenard Chamuriho amesema kuwa tayari mgogoro huo unaelekea ukingoni na muda wowote kuanzia sasa utapatiwa ufumbuzi na kuliachia eneo husika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi wa KADCO, Bw. Gregory Teu amesema kuwa kwa sasa kampuni imejipanga kuongeza wafanyakazi kulingana na mahitaji na kabla ya mwezi wa nane wakurugenzi ambao hawajathibitishwa watadhibitishwa ili kuongeza tija katika utendaji.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KADCO, Mhandisi Christopher Mukoma, amesema ukarabati wa kiwanja hicho ulihusisha sehemu ya maegesho ya ndege,ukarabati na uboreshaji wa mfumo wa maji safi na taka na uboreshaji wa jengo abiriaumeongeza idadi ya abiria kutoka laki tano kwa mwaka mpaka milioni 1.2 na kuweza kuhudumia ndege 11 kutoka ndege 6 kwa wakati mmoja.