News

ENG, NYAMHANGA AZINDUA MWONGOZO WA KUWAWEZESHA WAHANDISI WANAWAKE

Posted On: Tuesday 24, January 2017

Imeelezwa kuwa sababu za kihistoria, mila na desturi za jamii ni moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya ujenzi kwenye ushirikishaji wa wanawake katika utekelezaji wa miradi ya barabara nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi ),Eng. Joseph Nyamhanga wakati akizindua mwongozo wa kuimarisha ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara ambapo Serikali imekuja na mikakati mbalimbali ya kuwashirikisha wanawake katika miradi ya ujenzi wa barabara

"Maandalizi ya mwongozo huu ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika utekelezaji wa mikakati mbalimbali iliyojiwekea ili kuinua maisha ya wanawake kiuchumi,'' amesema Eng. Nyamhanga.

Eng. Nyamhanga ameongeza kuwa utekelezwaji wa mwongozo huo ni moja ya kichocheo cha kuwawezesha wanawake kutoa mchango mkubwa zaidi kuchumi nchini ambapo kwa sasa sekta ya ujenzi inachangia asilimia 13.6 kwenye pato la Taifa.

Aidha ametanabaisha kuwa kwa mwaka 2014/15 kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika miradi ya barabara wa uwiano wa kila wahandisi 100 wanaume wanawake 6 ambao kwenye usimamizi wa miradi uwiano ukiwa ni asilimia 6.

Kwa upande wake MKurugenzi wa Idara ya Barabara, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Ujenzi, Eng. Ven Ndyamukama amesema ushirikishwaji wa wanawake katika sekta ya ujenzi ulianza mwaka 1992 kwa kutekelezwa kwenye mikoa ya Mbeya, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Mtwara.

"Kama Wizara tuliona umuhimu wa kuanzisha kitengo maalum kwa ajili ya kuhakikisha tunawawezesha wanawake katika kazi za ujenzi na hili limesisitizwa hata kwenye sheria ya Ujenzi ya mwaka 2003 (CIP, 2003) kwa kuhakikisha wanawake wanashirikishwa katika kazi za ujenzi ili kuwainua kiuchumi' amesema Eng. Ndyamukama.

Ameongeza kuwa pamoja na mwongozo huu Wizara imeendelea kuwawezesha wanawake kwenye mafunzo mbalimbali ya ujenzi kupitia vyuo mbalimbali vilivyo chini ya wizara na taasisi binafsi.

Takwimu Kutoka Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB) na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) zinaonesha kwa mwaka 2014, kati ya jumla ya wahandisi 13,148 waliopo nchini wahandisi wanawake ni 926 ambao ni sawa na asilimia 6.5 wakati kati ya Makampuni ya makandarasi 8,071 yaliyosajiliwa ni makampuni 253 yanamilikiwa na wanawake sawa na asilimia 3.