News

ENG. NGONYANI AKAGUA UJENZI WA BARABARA MBANDE-KONGWA KM 11.71

Posted On: Tuesday 13, June 2017

Serikali imesisitiza nia yake ya kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Mbande-Kongwa yenye urefu wa KM 11.71 inayojengwa kwa kiwango cha lami unakamilika kwa wakati.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema hayo mkoani Dodoma jana, mara baada ya kukagua sehemu ya mradi wa barabara ya Mbande-Kongwa-Mpwapwa yenye urefu wa KM 49.14 ambao ujenzi wake unaendelea na kumuagiza Kaimu Meneja Wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Dodoma Eng. Salome Kabunda kusimamia mradi huo kikamilifu.

"Tutahakikisha fedha za mradi huu zinapatikana kwa wakati ili mradi ukamilikemapema ikiwa ni mkakati wa kuifungua wilaya hii na kuhuisha fursa za kimaendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Kongwa na Mpwapwa", amesema Eng. Ngonyani.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa za uwezekezaji katika maeneo hayo ikiwemo kurahisisha huduma za usafirishaji wa mazao kwa Wilaya hizo mkoani humo.

Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS, mkoa wa Dodoma Eng. Kabunda, amemhakikishia Naibu Waziri kuwa watamsimamia Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kwa karibu ili ubora wa barabara hiyo uendane na thamani ya fedha.

Aidha, Eng. Kabunda amewataka wananchi wa Wilaya ya Kongwa kushirikiana na mkarandarasi ili kuwezesha ujenzi huo kwenda kwa haraka.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw. Deogratius Ndejembi ameishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwani utachochea maendeleo wilayani humo.

Takribani shilingi Bilioni 7.5 zinatarajiwa kutumika katika sehemu ya kwanza ya mradi huo wa Mbande-Kongwa ambapo KM 5 zitajengwa na zinatarajiwa kumalizika ndani ya miezi nane.