News

DARAJA LA SELANDER KUWA MWAROBAINI WA FOLENI

Posted On: Friday 21, December 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa ujenzi wa Daraja jipya la Selander unatarajiwa kuwa mwarobaini wa kupunguza foleni ya magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi Jijini Dar es Salaam.

Amesema hayo leo katika eneo la Aga Khan jijini Dar es salaam wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo ambalo litaunganisha eneo la Aga Khan na Coco Beach jijini humo.

Rais Magufuli ameongeza kuwa msongamano wa magari katika maeneo mengi nchini huchangia kupoteza mapato ya nchi kutokana na watu wengi kupoteza muda mwingi barabarani kutokana na foleni.

"Daraja hili ni muhimu sana na likikamilika litasaidia kupunguza msongamano wa magari katika eneo hili, nchi yetu inapoteza takriban Bilioni 400 kwa mwaka kutokana na foleni", amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amemtaka mkandarasi anayejenga daraja hilo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa ubora na wakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amemhakikishia Rais Magufuli kuwa kufikia mwezi Januari mwakani mabasi yote 49000 yataanza kukatisha tiketi kwa njia ya kielektroniki kwa lengo la kudhibiti mapato.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) nchini, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa daraja hilo lina urefu wa mita 1,030 na upana wa mita 20.5 pamoja na njia 4 za magari, njia 2 za watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.

"Daraja hili ni kubwa kuliko madaraja yote nchini, litakuwa lina uwezo wa kubeba tani 180 kwa wakati mmoja na litadumu kwa muda wa miaka 100", amefafanua Mhandisi Mfugale.

Ameongeza kuwa ujenzi huo hautaathiri nyumba za watu wanaoishi katika maeneo hayo bali utapita kwenye hifadhi ya barabara.

Ujenzi wa mradi wa Daraja jipya la Selander utachukua muda wa miezi 30 kuanzia tarehe 23 mwezi Julai mwaka huu na unatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 256 ambazo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa ushirikiano wa Maendeleo ya kiuchumi (EDCF) na Serikali ya Tanzania.